Natafuta mwanamke mwenye utu, wema, uaminifu na tabia njema – sifa ambazo ataendelea kuwa nazo hata uzeeni. Sifa hizi zinaweza kubadilika kwa sababu ya maisha au kwa sababu ya mapenzi ya Mungu, lakini mabadiliko haya hayatakuwepo kwa haraka. Sura haidumu. Tabia hudumu. - Enock Maregesi
Maombi yako yasipojibiwa usikate tamaa, Mungu alishakusikia na tayari alishaandaa malaika wa kukuletea jibu. Jibu wakati mwingine huchelewa kufika kwa sababu ya nguvu za giza. Usiwe na haraka, muda wako ukifika utajibiwa. - Enock Maregesi
Kuna mafanikio ya aina mbili hapa duniani: Mafanikio ya Shetani na mafanikio ya Mungu. Mafanikio ya Shetani ni rahisi kupata na ni ya kitumwa. Mafanikio ya Mungu ni magumu kupata lakini ni ya hakika. Mungu akikubariki, pesa inaongezeka kama inavyoongezeka saa. - Enock Maregesi
Mungu alitengeneza familia. Alitengeneza koo, makabila na mataifa, ili watu wajuane na kuheshimiana. - Enock Maregesi
Mungu ndiye aliyetengeneza ubongo. Ni vizuri kuamini kwamba Yeye ndiye anayetupa maarifa, kupitia malaika wema, kuhusu maisha yetu na kuhusu siri ya uumbaji wake. - Enock Maregesi
Usipobadilisha maisha yako kuelekea kwenye takdiri yako utaishi kama Shetani anavyotaka, si kama Mungu anavyotaka. - Enock Maregesi
Akili yako isipokuwa timamu, familia itakushinda. Familia ikikushinda utalaumiwa na Mwenyezi Mungu. - Enock Maregesi
Ukitaka kujua maana halisi ya maisha yako kuwa tayari kufanya vitu vikubwa vitakavyohitaji nguvu ya Mungu kuvikamilisha – na kudumu katika maisha hayo kwa kafara ya maombi. - Enock Maregesi
Mawazo ya kukata tamaa yanaweza kusababisha tukamtengeneza au kumbuni tena Mungu kwa mfano wetu sisi wenyewe, mfano ambao kwa kawaida ni tofauti kabisa na mfano unaozungumzwa ndani ya Biblia. Hivyo tunaishia kutumikia mfano badala ya kumtumikia Mungu wa kweli. - Enock Maregesi
Ningependa – maisha yangu yatakapokoma hapa duniani – kukumbukwa kama mtu aliyejitahidi kwa kadiri ya uwezo wake wote, kutumia kipaji alichopewa na Mungu. - Enock Maregesi
Lengo la kuabudu ni kumtukuza, kumheshimu, kumsifia, kumfurahia, na kumpendeza Mungu. Ibada yetu lazima ionyeshe mapenzi ya kweli na uaminifu mkubwa kwa Mungu kwa ajili ya wema na rehema ambavyo ametupa kupitia Mwanaye wa Pekee aliyekufa msalabani, ili kutuokoa kutoka ubinafsini. - Enock Maregesi
Mungu ni mwandishi wa hadithi ya maisha yangu na ndiye anayeandika ukurasa wa mwisho. - Enock Maregesi
Watu hubariki wenzao ambao ni wakarimu, na hulaani wenzao ambao ni wabahili. Ukiwa mkarimu kwa watu umekopa neema kutoka kwa Mungu, na Mungu atakulipa kutokana na matendo yako. - Enock Maregesi
Usiifundishe familia yako anasa. Ifundishe upendo, unyenyekevu na hofu ya Mungu. Ukiifundisha anasa utahatarisha maisha ya mbinguni ya familia yako, na ya kwako pia. - Enock Maregesi
Mheshimu sana mtu aliyekupandisha juu kwa sababu utakaposhuka ndiye atakayekupokea, ijapokuwa unaweza usishuke kabisa au unaweza kushuka ukapokelewa na mtu mwingine baki, kwa kudura za Mwenyezi Mungu. - Enock Maregesi
Maamuzi ya Adamu na Hawa ya kutokumtii Mungu juu ya Mti wa Maarifa ya Mema na Mabaya, ndiyo yaliyosababisha Yesu Kristo ajitolee maisha yake ili wengine waweze kuishi. Hakuna Mungu bila Yesu. Mtafute Yesu, kukomboa sura na asili ya Mungu. - Enock Maregesi
Mungu alisema tupendane katika shida na raha; Luka 6:27-36. Katika matatizo mpende hasimuyo. Maumivu ya watu hufanana. - Enock Maregesi
Maisha tunayoishi ni mafupi, maisha ya mbinguni ni ya milele. Fundisha familia yako upendo na hofu ya Mungu, kwani hiyo ndiyo akili kushinda zote. Hekima ya kutunza familia inapatikana katika kitabu cha Mithali cha Agano la Kale. - Enock Maregesi
Kama nje ya uwezo wa kisheria ni uovu, hivyo basi, ndani ya uwezo wa kisheria ni wema. Kila mtu amepewa vipaji na Mwenyezi Mungu. Tumia vipaji vyako kutenda mema. Usitumie vipaji vyako kutenda maovu. - Enock Maregesi
Zawadi bora ya maisha kwa mwanadamu si fursa ya kufanya kazi kwa bidii na kuwa kitu fulani katika jamii. Ni amani ya Mungu katika moyo wa mwanadamu. - Enock Maregesi
Tumia kipaji ulichopewa na Mungu. - Enock Maregesi
Mungu alikupa vipaji ili uwanufaishe wengine na si kujinufaisha mwenyewe, na aliwapa wengine vipaji ili kukunufaisha wewe na si kujinufaisha wenyewe, kwa lengo la kuleta mabadiliko chanya katika dunia yetu. - Enock Maregesi
Matatizo ya watu yamekuwa makubwa kuliko Injili. Mungu hasisimuliwi na matatizo yako. Anasisimuliwa na imani yako. - Enock Maregesi
Kuzaliwa na kuishi ni mibaraka mikubwa ya Mwenyezi Mungu kuliko yote duniani. - Enock Maregesi
Mungu akikuweka mahali unapostahili kuwa, kulingana na takdiri ya maisha yako, hakuna mtu mwenye uwezo wa kushindana na kipaji chako. - Enock Maregesi
Kabbalah' ni sayansi ya Mti wa Uzima wa Milele wa Bustani ya Edeni au 'The Tree of Life of the Garden of Eden' katika mbingu ya nne, ambayo ni ramani ya ulimwengu na roho ya mwanadamu; au Sayansi ya Mungu, uchawi wa kujua 99% ya siri ya uumbaji wa Mungu. - Enock Maregesi
Kuikaribisha amani ya Mungu katika maisha yangu kumenisaidia. Naishi mbinguni duniani. - Enock Maregesi
Shetani ni mungu wa dunia hii kwa wale wasiomwamini Mungu. Kwa wale wanaomwamini Mungu, Mungu ndiye Mungu wa dunia hii. - Enock Maregesi
Mimi ni mwana wa Mungu. Sisi sote ni watoto wa Mungu. Lengo la kuzaliwa kwangu ni kufanya kazi pamoja na Roho Mtakatifu na malaika kumtumikia Bwana, na kueneza injili ya Yesu Kristo duniani kote, kupitia vitabu. - Enock Maregesi
Kuvunja sheria ni sawa na kufanya kosa, na kwa hiyo kuwa mkosaji, mbele ya sheria na mbele ya mungu. - Enock Maregesi
Hasanati ni matendo mema. Mema yanatoka kwa Mungu. Mabaya yanatoka kwa Shetani. Mke mwema anatoka kwa Mungu. Mke mbaya anatoka kwa Shetani. Mke mwema ana hekima na busara, ana maadili na tabia njema, ana utu na uchapakazi, ana wema na upendo, na ana aibu kwa wanaume. - Enock Maregesi
Mungu ni mwingi wa hekima, lakini kwa nini alimuumba Shetani? Kwa sababu, Shetani wakati mwingine ni hekima. Ukiendelea kupigwa, bila wewe kupiga, unaweza kuumia, familia yako inaweza kuumia pia! Kuepusha matatizo ya familia yako, wakati mwingine unahitaji kupigana. - Enock Maregesi
Wananchi wataendelea kuwepo hata kama serikali haitakuwepo. Serikali haiwezi kuwashinda wananchi. Sauti ya umma ni sauti ya Mungu. Serikali haiwezi kumshinda Mungu. - Enock Maregesi
Wengine hatuishi kama wafalme kwa sababu ya nguvu za giza – zilizopo kati ya Mungu na wanadamu. Nyota zetu zimefunikwa. Una kila kitu unachotafuta, ndani ya moyo wako. Usitafute furaha, utajiri au amani nje ya moyo wako. Tafuta furaha, utajiri au amani ndani ya moyo wako. - Enock Maregesi